Saturday, March 1, 2008

Wakimbizi wa Katumba kuanza kurejeshwa makwao Machi 9

Zoezi la kuwarejesha wakimbizi wa makambi ya Katumba na Mishamo wilayani Mpanda, mkoani Rukwa nchini mwao litaanza rasmi Machi 9, hadi Novemba, Mwaka huu.

Mgeni rasmi katika zoezi hilo anatarajiwa kuwa Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR).

Hayo yamo katika taarifa ya Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Bw. Thobias Mazanzala, kwa Waziri Mkuu Bw. Mizengo Pinda, katika ziara yake ya siku tatu wilayani Mpanda.

Aidha zoezi la kutoa uraia litaanza mara moja baada ya uzinduzi wa urejeshaji kuanza ambapo muda ulipangwa kwa wakimbizi wa makazi ya Katumba kurejea nchini Burundi ni Machi hadi Novemba mwaka huu ambapo kwa wakimbizi wa makazi ya Katumba ni Machi hadi Julai.

Bw. Mazanzala alifafanua kuwa kwa wakimbizi waishio katika makambi ya Katumba wamepewa muda mrefu wa kuondoka kutokana na uwingi wa waliojiandikisha.

Alisema kuwa makazi ya wakimbizi ya Katumba yana watu 109,243 ambapo makazi ya Mishamo yana wakimbizi 56,251 na zoezi la maandalizi la kuwasajili wakimbizi wote wanaotaka kurejea burundi na wanaotaka kubaki Tanzania na kuomba uraia lilifanywa kwa ushirikiano wa UNHCR na serikali ya Tanzania na ya Burundi.

Alifafanua kuwa jumla ya familia 23,527 za makazi ya katumba yenye wakimbizi 108,925 waliosajiriwa ambapo wakimbizi 35,000 sawa na asilimia 35 ndio waliokubali kurejea nchini kwao kwa hiari na asilima 3 kutochagua chochote.

Alisema kuwa katika makazi ya Mishamo jumla ya wakimbizi 1500 kati ya 56,251 ndio waliokubali kurejea nchini kwao kwa hiari.

SOURCE: Nipashe

No comments: