Tuesday, March 11, 2008

JOHN Nolan, yule raia wa Ireland aliyejaribu kuighilibu Serikali ya Tanzania imruhusu aanzishe mashamba ya kamba (prawns) ambayo yangeiharibu kabisa Delta ya Rufiji, alipata kuliambia gazeti moja la Uingereza kwamba kati ya nchi za "ajabu" alizopata kuishi ni Tanzania .

Nolan aliliambia gazeti hilo ya kwamba Tanzania ndiyo nchi pekee duniani ambayo Mzungu anaweza kuingia akiwa na dola tano tu mfukoni na akaondoka miaka mitano baadaye akiwa milionea! Alitoa mfano wa yeye mwenyewe kwamba aliingia Tanzania akiwa hana kitu, lakini 'akatengeneza pesa' akiwa katika chumba chake cha hoteli kutokana na dili walizochonga na viongozi ambao walimwamini kwa kuwa tu ni Mzungu!Lakini Nolan si mgeni pekee aliyepata kuikejeli Tanzania .

Mwaka jana gazeti la Mtanzania lilipata kumnukuu mwekezaji mmoja kutoka China , anayefanya biashara ya kuuza kamba na kambakochi Mashariki ya Mbali, akiikejeli Tanzania kwamba rushwa yake ni "poa".

Kwa mujibu wa Mchina huyo, ni katika Tanzania tu ambapo unaweza kumwita hakimu nyumbani kwako na kumpa rushwa ya Sh. 100,000 tu, na kisha kumpa maelekezo ya namna ya kutoa hukumu ya kesi ya mamilioni ya pesa inayokuhusu!Lakini kama utashangaa na kutoziamini kauli hizo za Nolan na za Mchina huyo, utasemaje kuhusu hii ya Rais mstaafu, Benjamin Mkapa kuanzisha kampuni yake ya biashara (ANBEM) yeye na mkewe, mwaka 1999, akiwa bado Ikulu?. Kwa kufanya hivyo, Mkapa akawa Rais wa kwanza katika historia ya Tanzania kufanya biashara akiwa Ikulu. Historia bwana, nani hapendi kuweka historia ya ujasiriamali?Lakini hakuishia hapo.

Mwaka mmoja kabla ya kuondoka madarakani; yaani Desemba 29, 2004, Mkapa huyo huyo akashirikiana na aliyekuwa Waziri wake wa Fedha na baadaye Nishati na Madini, Daniel Yona, kusajili kampuni nyingine binafsi iitwayo Tanpower Resources Company, na akaisimamia kununua asilimia 85 ya uliokuwa mradi wa umma wa makaa ya mawe wa Kiwira mkoani Mbeya.Lakini pia hakuishia hapo.

Akautumia wadhifa wake wa urais kuhakikisha kampuni yake hiyo mpya – wakurugenzi wakiwa ni pamoja na mkewe na mtoto wake, kuingia mkataba wa kuiuzia Tanesco megawati 200 za umeme katika gridi ya taifa.Raia wema waliohoji iwapo hakuna mgongano wa maslahi kwa Rais kufanya biashara akiwa bado Ikulu; huku akinunua kampuni ya umma (Kiwira) na kuingia mkataba wa kibiashara na kampuni nyingine ya umma (Tanesco), walinyamazishwa haraka kwa kuambiwa Mkapa ni "mjasiriamali" , na kwamba anaonyesha "ujasiriamali" kwa vitendo akiwa Ikulu! Upo hapo?