Saturday, March 1, 2008

Bilioni 50/- zarejeshwa 2008-03-01 09:01:31 Na Mwandishi Wetu

Zaidi ya Sh. bilioni 50 kati ya bilioni 133 zilizochotwa na mafisadi kupitia akaunti ya madeni ya nje ya Benki Kuu (BoT) zimerudishwa serikalini.

Pamoja na fedha hizo, mali nyingine za watuhumiwa hao zilizoko nje na ndani ya nchi zikiwemo nyumba zimegundulika kwa mujibu wa Waziri wa Fedha na Mipango, Bw. Mustapha Mkulo.

Bw. Mkulo alitaja kiwango hicho kwenye mkutano wa waandishi wa habari, uliofanyika jana jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Timu ya Maofisa wa Shirika la Fedha Duniani (IMF) na kushirikisha maofisa kadhaa wa wizara hiyo na BoT.

Waziri aliyekuwa anajibu maswali ya waandishi wa habari alisema mali hizo zimenaswa katika kipindi cha mwezi mmoja na lengo ni kurudisha fedha zote, kukamata mali za watuhumiwa na kuwachukulia hatua za kisheria.

Alipoombwa kutaja majina ya wahusika na kampuni zao Bw. Mkulo alisema kwa sasa si wakati muafaka kwani kutavuruga upelelezi na jitihada za kurudisha fedha hizo na kuwafikisha mbele ya sheria watuhumiwa.

Tume iliyogundua mali hizo ni ile iliyoundwa na Rais Jakaya Kikwete , mwezi uliopita inayoongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw. Johnson Mwanyika na wajumbe wengine kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) kwa kushirikiana na Bodi ya Wakurugenzi wa BoT.

Tume hiyo imepewa kazi ya kurudisha mali na fedha za watuhumiwa na kuwachukulia hatua za kisheria wahusika.

Makampuni 22 yaliyotuhumiwa kulipwa Sh. bilioni 133 na BoT kinyume cha sheria katika kipindi cha 2005/06 kupitia akaunti ya EPA ni pamoja na Bencon, VB & Associates, Bina Resorts, Venus Hotel, Njake Hotels and Tours, Maltan Mining Companies, Money Planners &Consultants.

Mengine ni Bora Hotels and Apartments, BV Holdings , Ndovu Soap, Navy Cuts Tobacco, Changanyikeni Residential Complex, Kagoda Agricultre, G&T International, Excellent Services, Mibale Farm, Liquidity Service, Clayton Marketing, M/S Rastash, Maregesi Law Chamber (Advocates), Kiloloma & Brothers, Karnel Ltd.

Makampuni hayo yalilipwa baada ya kuwasilisha vielelezo vya kughushi, hati batili na baadhi hayakuwa na nyaraka zozote na kwa ujumla hayakustahili kulipwa chochote.

Makampuni hayo yaliibuliwa na kampuni ya Ernst & Young ya Uingereza iliyopewa zabuni na serikali kuchunguza madai ya upotevu wa mabilioni ndani ya BoT kupitia akaunti ya madeni ya nje (EPA).

Katika mkutano huo, Waziri Mkulo, alisema majadiliano kati ya serikali na maofisa wa IMF yalilenga kwenye usimamizi na utunzaji wa fedha. `

`Tumezungumzia hali ya uchumi na kuazimia kuweka mkazo katika kukuza uchumi katika kiwango cha juu na cha chini.`` ``

Kadhalika tumeazimia kuboresha na kusimamia ipasavyo ukusanyaji mapato ili kuliondosha taifa na utegemezi na umaskini,`` alisema.

Alisema pamoja na hayo serikali imeazimia kuimarisha sekta ya nishati mijini na vijijini ili kuondoa matatizo yasiyokwisha ya nishati.

Waziri alisema mazungumzo hayo yaliazimia pia kuwa lazima Tanzania izingatie utawala bora unaofuata sheria.


SOURCE: Nipashe

No comments: