Mbunge huyo alidai bungeni jana kuwa mwaka 2004, Mkapa kwa kushirikiana na mkewe pamoja na Yona, walianzisha Kampuni ya TanPower Resources Ltd na mwaka mmoja baadaye wakauziwa machimbo ya Kiwira kimya kimya.
Kimaro alitoa madai hayo alipokuwa akichangia Muswada wa Sheria ya Umeme wa Mwaka 2008, bungeni, mjini hapa juzi jioni.
Alidai kuwa katika mauziano hayo ya siri, Kampuni ya TanPower Resources Limited,
ilikuwa iilipe serikali Sh700milioni katika mradi huo uliogharimu, zaidi ya Sh4bilioni, lakini kampuni hiyo ilifanya malipo ya awali ya Sh70milioni tu.
"Waliuziwa kwa Sh700milioni bila kutangazwa na wao wakalipa down payment (malipo
ya awali)Sh70 milioni," alisema Kimaro.
Aliendelea kudai kuwa mwaka 2006, Mkapa, Anna na Yona, waliingia mkataba na Shirika la
Umeme nchini (Tanesco) kwa ajili ya kufua umeme kwa makubaliano ya kulipwa Gharama za uwekezaji ('capacity charge') Sh146milioni kila siku, bila kujali kwamba wamefua umeme au la.
"Sasa mimi nauliza huu ni uadilifu kweli? Haya ni maadili kweli? Tufike mahala
tuseme inatosha. Hivi tunawafundisha nini vijana hawa ambao ni mawaziri?," alihoji
Kimaro na kuongeza:
"Rais Jakaya Kikwete alisema urais wake hauna ubia na mtu. Basi aseme huu ni mwisho kwa wanaotuhujumu, tuwaambie basi na washughulikiwe kwa mujibu wa sheria."
Awali, akichangia muswada huo, Kimaro alisema ipo haja ya kuwa makini katika kuupitisha muswada huo kwa kuwa wawekezaji watakaokuja kuwekeza katika umeme, si rahisi kwenda vijijini kusambaza nishati hiyo.
Kutokana na hali hiyo, aliitaka serikali kuifufua Tanesco kwa kuipa fedha ili (serikali) iwe na chombo chake cha kuzalisha umeme.
Naye Mbunge wa Mpanda Kati (Chadema), Said Amour Arfi, alishangazwa namna serikali
inavyotumia nguvu nyingi kuupitisha muswada huo.
Alisema haafiki kupitishwa kwa muswada huo na kuongeza kuwa nguvu inayotumika kuharakisha kupitishwa muswada huo si ya kawaida.
Alisema hoja ya kuwa muswada huo ukipita, wananchi wa vijijini watapata umeme wa bei rahisi, haina nguvu.
Alitoa mfano wa Kampuni ya Artumas ambayo baadhi ya wabunge waliipigia debe, kwamba haitaweza kuondoa matatizo ya umeme.
Tanesco itaingiaje katika ushindani wakati ikiwa hoi? Tanesco inavishwa majukumu
ya kisiasa,? alisema na kuonya kwamba wawekezaji watakaokuja si ajabu wakafanana na hadithi ya ubinafsishwaji wa Benki ya NMB.
Alikumbusha kuwa wakati NMB inabinafsishwa, ilisemwa kuwa itakuwa benki ya wananchi
na itawafikia watu wengi, lakini leo hii ukitaka kufungua tawi vijijini wana vigezo vyao na si jambo rahisi kufika huko.
?Na hao (wawekezaji) wakija, wataweka vigezo vyao vya kusambaza umeme vijijini ambavyo havitawawezesha wananchi wa huko kunufaika na huduma hiyo,? alibainisha.
Naye Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela alimwangaliza Waziri wa Nishati
na Madini, William Ngeleja, kutambua aina ya wawekezaji wanaotarajiwa kuwekeza katika sekta ya umeme baada ya sheria mpya ya sekta hiyo kupitishwa, kwani ndiyo watakaomwangusha ama kumwinua.
?Nakupa angalizo Mheshimiwa Waziri, ujue kuwa aina ya wawekezaji watakaoingia katika sekta ya nishati ndiyo watakaokuangusha au kukuinua, wapo Watanzania wenzetu wanajiandaa kuingia katika biashara hiyo, wengine ni wale walionufaika na mikataba mibovu kama ule wa Richmond,? alitahadharisha Mbunge huyo.
Alidai kuwa baadhi ya Watanzania, hususani walionufaika na mikataba inayolitia hasara Tanesco, wameanza kujiandaa kuwekeza kwenye sekta hiyo.
Alisema kuwa, kimsingi ni muhimu kwa serikali kuhakikisha kuwa Tanesco inakuwa imara katika kipindi hiki cha ushindani, ambacho kinahitaji nguvu zaidi kwa shirika hilo la umeme ili kukabiliana na ushindani utakaotokana na kupitishwa kwa sheria hiyo.
Aliangaliza kuwa serikali inatakiwa kutambua kuwa Mtanzania wa leo anaitambua nchi yake na hivyo kuna umuhimu mkubwa kuwa na ufahamu kwamba mageuzi ya kiuchumi ni muhimu na sharti yajengwe palipo na mfumo imara wa usambazaji wa umeme.
Kwa upande wake Mbunge wa Moshi Mjini (Chadaema), Philemon Ndesamburo ambaye mbali
ya kuunga mkono hoja hiyo alishauri kuwa umeme usiwe kitu cha anasa na badala yake kiweze kupatikana kwa kila mtu anayekihitaji.
Mbunge huyo wa Moshi Mjini alishauri kuwa pamoja na umuhimu wa serikali kuingia katika mfumo huo mpya, jambo muhimu ni kuhakikisha kuwa maeneo ya mipakani yakatumia fursa ya kuwepo umeme kutoka nchi jirani.