Thursday, February 14, 2008


“Kumbadili waziri, hata Waziri Mkuu, si jambo la ajabu. Anaweza kujiuzulu, anaweza kufukuzwa, na nchi isitikisike. Lakini huwezi kumtikisa Rais wa nchi bila kuitikisa nchi yenyewe. Ni vizuri jambo hili likatamkwa waziwazi na likaeleweka sawa sawa. Maana watu wengine wananong’ona nong’ona kuwajibika kwa Rais kana kwamba ni jambo la mchezo mchezo tu.
Kulazimika kumchukulia hatua Rais wa nchi ni mkasa na balaa kwa nchi yoyote ile. Ndiyo maana tunatakiwa kuwateua na kuwachagua marais wetu kwa uangalifu mkubwa, na ndiyo maana wakisha kuchaguliwa, wanatakiwa kujiheshimu na kuwa waangalifu sana.” - Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
LAZIMA nikiri kuwa niliyakumbuka maneno haya mara tu baada ya Edward Ngoyai Lowassa, kutangaza kuwa alikuwa amewasilisha barua kwa Rais Jakaya Kikwete, ya kutaka kujiuzulu wadhifa wake wa Waziri Mkuu, kutokana na kuhusishwa na kashfa ya Richmond.
Maneno hayo yamo katika kitabu cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kiitwacho “Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania.” Mwalimu alikiandika kitabu hiki, nusu ya mwanzo ya miaka ya ‘90, baada ya nchi kutikiswa na mambo matatu makubwa: Mosi, ilikuwa ni hatua ya Zanzibar kujiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC). Pili ilikuwa ni utaratibu mpya wa kumpata Makamu wa Rais, yaani chini ya mfumo wa vyama vingi. Na tatu ni wabunge wa Tanzania Bara walipodai serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano.
Kwa hiyo, inatosha kusema tu kwamba, kwa kiasi kikubwa, niliposikia uamuzi wa Lowassa, nilikikumbuka kitabu hicho. Sitazungumzia suala la Richmond katika makala hii. Lakini ninataka kuwasilisha mtazamo wa Mwalimu Nyerere kuhusu suala la wakubwa kujiuzulu kwa hiari pale wanapokoroga mambo au mambo yanapoelekea kuwakoroga.
Nilipoangalia kwa makini Mwalimu anajikita zaidi kwa nafasi za mawaziri na Waziri Mkuu, ambao wanapaswa kuachia ngazi pale mambo yanapovurugika chini ya usimamizi wao.
Watu wengi wamesikika wakisema kwamba tamko la Lowassa la kujiuzulu uwaziri mkuu, lilikuwa limeitikisa nchi. Inawezekana. Lakini kwa mtazamo wa Mwalimu Nyerere, “kumbadili waziri, hata Waziri Mkuu, si jambo la ajabu. Anaweza kujiuzulu, anaweza kufukuzwa, na nchi isitikisike. Lakini huwezi kumtikisa Rais wa nchi bila kuitikisa nchi yenyewe.” Kwa mtazamo huo wa Mwalimu, nchi inaweza tu kutikisika endapo tu Rais ataguswa.
Mara nyingi suala la kujiuzulu kwa mawaziri au hata Waziri Mkuu, limekuwa ni suala la vuta nikuvute. Waziri anaweza kuhusishwa na kashfa fulani, lakini zinapokuja hoja za kutaka ajiuzulu, anakuwa kama hasikii kitu.
Pengine mfano pekee katika historia ya nchi hii, (ukiondoa huu wa Lowassa), ni ule uliomhusu rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi. Akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, watumishi walioko chini ya wizara yake, huko Shinyanga, walisababisha vifo vya mahabusu. Ilibidi aachie ngazi kwa hiari yake, na hatua hiyo ilimjengea heshima.
Katika kitabu chake, “Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania”, Mwalimu Nyerere anasema: “Pengine inafaa niseme kwamba inashangaza na kutisha kidogo, kuona kuwa kujiuzulu kwa waziri yeyote kunafanywa kuwa ni jambo la kuvutana au la kubembelezana.
“Ndugu Ali Hassan Mwinyi aliwahi kuwaa Waziri wa Mambo ya Ndani katika Serikali ya Muungano. Makosa fulani yalifanyika katika wizara yake. Hakuwa amefanya yeye, yalikuwa yamefanywa na watendaji fulani walio chini ya wizara yake. Alilazimika kubeba lawama, akajiuzulu. Nadhani kuna wengine waliolazimika kujiuzulu kutokana na mkasa huo huo.”
Huo ndio msimamo wa Mwalimu kuhusu dhana ya uwajibikaji, hata kama mhusika hakushiriki kutenda kosa, ili mradi tu dosari imefanyika chini ya dhamana yake.
Lakini pia Mwalimu anazungumzia suala la kumbadilisha Waziri Mkuu, kuwa si kitendo cha ajabu. Na hapa anarejea mfano wa jinsi alivyomwondoa Waziri Mkuu, Rashidi Kawawa na kumwingiza Edward Moringe Sokoine. Mwalimu anazungumzia tukio hilo kwa maneno yafuatayo:
“Wala kubadili Waziri Mkuu si jambo la ajabu. Ndugu Rashidi Mfaume Kawawa alikuwa ni Waziri Mkuu wangu kwa muda mrefu. Hakuwa amefanya kosa lolote; lakini nilitaka kumbadili na kuteua Waziri Mkuu mwingine. Nilimwita, nikamwambia hivyo. Tukakaa pamoja mimi na yeye, tukashauriana na kukubaliana ni nani anafaa kushika nafasi yake. Nikamteua Edward Moringe Sokoine. Najua kuwa watu wa aina ya Rashidi Kawawa ni adimu sana duniani, hawazaliwi kila siku.
“Ni jambo la kushangaza kidogo kwamba viongozi…wanaona kuwa ni kosa kuwakumbusha kuwa vyeo walivyo navyo ni dhamana. Wanadhani kuwa uwaziri ni usultani: ukishakuwa sultani utakufa ukiwa sultani! Nadhani wanakosea. Nchi hii imewahi kung’oa masultani wa kila aina. Tukianza kuvumilia masultani wa kuchaguliwa tutapanda mbegu ya masultani wa kuzaliwa.”
Hata hivyo, pamoja na mtazamo wake kuhusu kujiuzulu, Mwalimu Nyerere anarudi nyuma kuhusu ugumu wa kudhibiti makosa yasitendeke katika mchakato mzima wa utendaji kazi. Kwamba huwezi kujijengea utaratibu wa kuzuia kabisa makosa yasifanyike. Lakini anasema kwamba yakifanyika hakuna budi wahusika wawajibike. Namnukuu:
“Hatuwezi kujijengea utaratibu wowote ambao utazuia kabisa makosa yasifanyike, hata makosa makubwa. Lakini tunatazamia kuwa yakifanyika, wanaohusika watawajibika.
“Na katika makosa makubwa ya maadili na utendaji, mwenye jukumu la wazi wazi la kuwadhibiti wahusika ni Rais. Mawaziri wake wanapofanya makosa makubwa, na badala ya kujiuzulu waanze kufanya hila na kutafuta visingizio vya kutofanya hivyo, ni wajibu wa Rais kuwafukuza, na tunamtazamia kufanya hivyo.
“Ni kazi yake mwenyewe, asiyoweza kusaidiwa na mtu mwingine. Mtu anaweza kumsaidia Rais kumnong’oneza waziri wake kujiuzulu, lakini hawezi kumsaidia kufukuza waziri wake. Hiyo ni kazi ya Rais peke yake. Asipoifanya, kosa ni lake peke yake.”
Kwa mantiki hiyo, mawaziri waliojiuzulu sambamba na Waziri Mkuu, Edward Lowassa, yaani aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, na Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dk Ibrahim Msabaha, wangeweza kuondolewa tu na Rais pekee endapo wasingetamka kuachia ngazi zao kwa hiari.
Na kama mawaziri hao wawili wangebaki kimya na Rais naye akanyamaza, basi hakuna mwingine zaidi ambaye anaweza kuingilia kati, isipokuwa tu manung’uniko na minong’ono ya hapa na pale mitaani.
Pengine jambo la msingi ambalo limeleta mabadiliko makubwa ya uongozi wa Awamu ya Nne wiki iliyopita ni pale wachache walipopiga moyo konde na kuuweka pembeni woga. Na hapa naweza kurejea wajumbe wa Kamati ya Bunge, iliyochunguza kashfa ya Richmond.
Nasema waliweka woga pembeni kwa kuwa mmoja wa viongozi waliyekuwa wakimgusa katika uchunguzi wao alikuwa ni Waziri Mkuu. Hapa palihitaji kupiga moyo konde kweli kweli.
Lakini pia kulikuwa na ujasiri upande wa wabunge. Ujasiri wao huo ulianza pale walipoikataa semina ya Wizara ya Nishati na Madini, ambayo ilikuwa iegemee kwenye suala la Richmond.
Nasema huu ni ujasiri kwa kuwa kumekuwa kukisika kauli za mara kwa mara, kwamba Bunge letu ni rubber stamp, yaani ni mhuri tu wa kupitisha matakwa ya Serikali. Bahati nzuri wabunge wameapa kuwa kitu kimoja katika masuala yanayohusu maslahi ya taifa.
Mwalimu katika kitabu chake anakemea suala la woga. Anasema: “Kukubali kufanywa vikaragosi vya viongozi ni dalili ya woga. Si dalili ya heshima. Na woga na heshima ni vitu viwili mbali mbali. Maadili mema yanatutaka tuheshimu viongozi wetu, madhali wanajitahidi kutimiza wajibu wao.
“Maadili mema hayatudai tuwaogope viongozi wetu. Na viongozi makini hupenda kupata heshima ya wananchi wenzao, lakini hawapendi kuongopwa. Kuogopwa ni sifa na ada ya madikteta. Viongozi halisi hawapendi kushiriki. Kujenga mazoea ya kutii viongozi, hata katika mambo haramu ni dalili ya woga, ni kukaribisha udikteta.”
Edward Lowassa kaachia uwaziri mkuu. Nazir Karamagi kaachia uwaziri wa Nishati na Madini na Dk Ibrahim Msabaha kaachia nafasi kama hiyo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kwa kiasi fulani, nadhani, Mwalimu anaweza kuwa anageukageuka kwa furaha kaburini kwake kutokana na uamuzi wao na matarajio yake.


kwa kweli huyu Mheshimiwa Harrison Mwakyemebe na kamati yake ninawaheshimu sana kwa jinsi walivyofanya kazi hii.

Je, Mnakumbuka!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!akiapa kuilinda Katiba alipoapishwa kuwa Waziri Mkuu

Pichani Waziri Mkuu Bw. Edward Lowassa (CCM)
Hatimaye mchawi wa Richmond ni yule ambaye watu walimhisi kwa muda mrefu. Na sasa tumegundua hakuwa peke yake. Taarifa ya leo ya Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa mwishoni mwa mwaka jana kuchunguza mkataba wa Richmond imeonesha kuwa siyo tu taratibu zilikiukwa bali pia kuna ushahidi mkubwa wa rushwa


Ripoti hiyo ambayo inaonesha wazi kuwa mhusika mkubwa wa sakata hili zima ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa vile bwana Lowassa aliapa kuilinda na kuitetea Katiba yetu na kwa vitendo vyake ameshindwa kufanya hivyo hana budi kuwa wa kwanza kuwajibika yeye mwenyewe bila ya kungojea kuwajibishwa. Mhe. Lowassa kwa hili umekosea na liwe somo kwa viongozi wengine wote kuwa Tanzania inabadilika na viongozi wasioongoza hawana budi kuwekwa pembeni. Mhe. Lowassa tunataka ujiuzulu wadhifa wako mara moja


Pamoja na wewe wahusika wengine wote ambao wanatajwa katika ripoti hiyo akiwemo Waziri Msabaha, Karamagi, Rostam Aziz na Mwanyika nao pia wajiuzulu mara moja kwa kutumia madaraka yao vibaya, kulidanganya Taifa, kufanya kazi kinyume na maadili, na kwa kuliletea Taifa letu hasara.


Watanzania wana mambo mengine ya msingi ya kufuatilia (kama BoT na mengine) na wakati umefika suala la Richmond lifikie kikomo kwa viongozi na wahusika wote kujiuzulu. Tulishasema toka awali kuwa Baraza hili la mawaziri ni la kishikaji na ambalo limemwangusha sana Rais na kwa hakika ni kujiangusha alikojitakia kwani alishaonywa, halina budi kuvunjwa ili Baraza jipya litakalokidhi hamu na matamanio ya Watanzania na ambalo wajumbe wake watatoka hata nje ya CCM liundwe ili tuendelee na jitihada za kulijenga Taifa letu


14/2/....... nisiku maarum kwa watu wapendanao (familia, Marafiki) nisiku ambayo hasa hasa husherekewa na Vijana lika kati ya 14-25 ndio huwa na moto sana. Valentine sio ngono ila watu wanaipeleka kuwa ngono kwa kufanya mambo yasiyostahili kitu kina jenga hisia mbaya kwa jamii. Nawashauri siku ya leo 14/2/2008 jitahidi kuangaria wapi hukuwa sawa ktk mahusiano either ya Mume& Mke (Familia kwa ujumla + watoto), Jamii inayokuzunguka, na Marafiki jirudi na uanze upya niwakati wa kupanga na wenzi wako.


Catherine & Shumbusho wanawatakia watanzania wote Heri ya Wapendanao


JK akiteta jambo na Waziri Mkuu Mpya pamoja na Makamu wake.

Unaweza kuwemo!

Baraza jipya la mawazili


Rahisi wa Jamuhuli ya Muungano wa Tanzania akiwa na makamu wa rais d. ali mohamed shein na waziri mkuu mh. mizengo pinda pamoja na baraza jipya la mawaziri baada ya kuliapisha leo ikulu ndogo ya chamwino, dodoma