Tuesday, February 12, 2008

MAONI YA WANAHARAKATI KUHUSU RIPOTI YA RICHMOND ILIYOWASILISHWA BUNGENI DODOMA 06/02/08

MAONI YA WANAHARAKATI KUHUSU RIPOTI YA RICHMOND ILIYOWASILISHWA BUNGENI DODOMA 06/02/08

Wanaharakati wa masuala ya Jinsia, Haki za Binadamu na ukombozi wa wanawake kwa pamoja tunawapongeza wabunge wa Bunge la Jamhuri la Muungano wa Tanzania hususan walioanzisha hii hoja nzito na kuibua mjadala mzito wa Kitaifa, Kamati Teule, Vyama vya siasa, vyombo vya habari na wanaharakati wote kwa kuonyesha uzalendo juu ya mali za Taifa la Tanzania kwa kuweza kufichua na kuweka wazi mkataba wenye utata wa Richmond.

Pia tunawapongeza kwa kuona dalili kuwa Bunge limeanza kurudisha hadhi yake na tunatambua kuomba radhikulikofanywa na Spika wa Bunge kutokana na kauli yake kutumia neno ‘kukurupuka’ dhidi ya Naibu Spika wa Bunge
Tunalitaka Bunge lisirudi nyuma bali liendelee kusonga mbele kutetea na kusimamia maslahi ya wananchi

Sisi wanaharakati tunadai yafuatayo:
· Ripoti ya Kamati Teule ya Mkataba wa Richmond ichukuliwe kwa uzito wake kama ilivyo na iheshimiwe.
· Wahusika wote waliotajwa ( iwe Taasisi au mtu mmoja mmoja ) wawajibishwe kulingana na misingi ya Katiba na Sheria.
· Liundwe baraza jipya la mawaziri kufuata maadili ya uongozi
· Mikataba mipya inayotarajiwa kusainiwa iwe wazi na shirikishi
· Kamati ya Rais ya madini na ya BoT zibadilishwe na kuundwa kwa Kamati za Bunge za kuchunguza masuala ya madini, BoT pamoja na masuala yote ya raslimali za Taifa hili hususan katika vipindi vya urekebishaji wa uchumi.
· Mikataba yote yenye utata ifuatiliwe upya na iwe wazi
· Taasisi ya kudhibiti na kuzuia rushwa (TAKUKURU) iwe chini ya Bunge la Jamhuri ya Tanzania
· Mali yote ya Taifa iliyopotea irejeshwe
· Turejee ripoti ya Warioba ya mwaka 1996 kama kweli tunahitaji kupingana na ufisadi wowote ule
· Tunatoa angalizo kwa Spika wa Bunge kwamba masuala yote nyeti yalenge maslahi ya wananchi na sio maslahi ya mtu mmoja mmoja au kikundi fulani

Mwisho, Suala hili linatoa changamoto kwa mfumo mzima wa demokrasia nchini. Mfumo tulionao wa demokrasia wakilishi haufai tunadai demokrasia shirikishi.

07/02/08

No comments: