Wednesday, March 26, 2008

Vyama korija, demokrasia sufuri

RAI YA JENERALI


NIMEKWISHA kueleza huko nyuma jinsi Mwalimu Julius Nyerere alivyotaka Chama cha Mapinduzi (CCM) kigawanyike ili viwepo vyama viwili vyenye nguvu karibu sawa ingawa vikitofautiana kuhusu masuala ya itikadi, sera na mbinu za utekelezaji.

Mantiki ya mtazamo wa Mwalimu ilijengeka juu ya uelewa aliokuwa nao kuhusu siasa za ushindani. Kwa mtazamo wake, hakuna maana ya kuwa na mfumo unaoitwa wa “vyama vingi” lakini wakati huo huo ukajenga utaratibu ambao hauruhusu upinzani wa maana.

Nyerere hakufanikiwa katika hilo, na chama chake kikaendelea kuwa kimoja na chenye nguvu kubwa miongoni mwa jamii. Umoja huu na nguvu hiyo havitokani na makubaliano ya kiitikadi wala maelewano au mwafaka kuhusu masuala makuu ya kitaifa.

Ukweli ni kwamba hakuna makubaliano ya kiitikadi kwa sababu katika chama kisichokuwa na itikadi kuu si rahisi kupata ukinzani kwani ukinzani huzuka kutokana na itikadi inayobishiwa na kundi fulani, na bila ukinzani haiwezekani yakawapo makubaliano.

Hali kadhalika, kwa mwafaka kuhusu masuala makuu ya kitaifa. Kiongozi mmoja wa chama hicho aliwahi kusema, mara tu baada ya uchaguzi kwisha, kwamba ilani ya chama chake, ambayo ndiyo ilipelekwa kwa wananchi wakamchagua, haitekelezeki. Maana halisi ya tamko lake hilo ni kwamba ilani ni ujanja unaobuniwa wa kuwazuga wapiga kura kwa kuwahadaa na ahadi nyingi ambazo hao wanaozitoa wanajua fika kwamba hawana nia ya kuzitimiza.

Kama hiyo ni kweli, basi hakuna njia ya kupata mwafaka kuhusu suala lo lote la kitaifa, kwa sababu hata hayo tuliyoyaorodhesha kwamba ni mambo yatakayopewa kipaumbele ni kiinimacho tu. Katika hali kama hiyo programu huzuka kutegemea na viongozi wakuu wanavyojihisi kwa wakati huo, na utekelezaji huwa daima ni wa zima-moto. Hapo haiwezekani kuwa na mwafaka wa kiutaratibu wala ukinzani ulioaratibiwa.

Kimsingi, Chama cha Mapinduzi kimeendelea kuwa kimoja kwa sababu bado kiko madarakani, na kimekuwa kikitumia madaraka ya dola kuendesha kazi zake za kichama. Mifano michache inaweza kusaidia kueleza ninachokisema hapa:

Mheshimiwa Rais wa Jamhuri anapopanda ndege ya Serikali kwenda mikoani kukagua miradi ya maendeleo, na akiwa huko akaendesha mikutano ya chama chake, tunaweza kusema kwamba chama chake kinakuwa kimepokea ruzuku kutoka serikalini kwa maana ya usafiri, malazi, chakula, na vinywaji. Aidha, katika misafara hiyo anaambatana na maofisa kadhaa wa chama chake, ambao nao hudandia ‘takrima’ iliyoandaliwa kwa ajili ya Rais.

Hali ni hiyo hiyo inapoandaliwa ziara ya Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Rais wa Zanzibar, Waziri Kiongozi na mawaziri wa kila aina, pamoja na wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya. Zaidi ya hayo tuongeze utaratibu unaotumika wa kuwateua maofisa waandamizi wa chama-tawala kuwa mawaziri wanaolipwa na Serikali, wanaosafiri kwa magari ya Serikali, n.k.

Tungeweza kupiga mahesabu yaliyotulia tungegundua kwamba Serikali ya Tanzania inatoa ruzuku kwa CCM bila kukiri hivyo. Na tukumbuke kwamba ruzuku hii ni mbali kabisa na ile inayotolewa kwa kila chama kulingana na wingi wa kura kilizopata katika uchaguzi wa Rais na wingi wa wabunge wa chama husika, huko nako chama-tawala kimetwaa mgao wa simba.

Hivi sasa iko minong’ono ambayo haikosi chembe ya ukweli kwamba hata baadhi ya masuala yanayoibuka kuhusu ‘ufisadi’ katika asasi nyeti za Taifa yametokana na chama-tawaka kuchotewa fedha kutoka asasi hizo kwa ajili ya kampeni za uchaguzi. Ni dhahiri kwamba chama hicho kimeegemea mno Serikali kiasi kwamba ni vigumu kukifikiria kikiendelea kuwapo iwapo, kwa sababu yo yote ile, kingepoteza madaraka.

Kikiwa kinaendelea kuwa madarakani kitaendelea kuvuta kila aina ya watu, wema na waovu, waongofu na mafisadi, wazalendo na wahaini, alimradi chama bado ni chimbuko la neema, ndicho kitovu cha mgawanyo wa madaraka ya dola katika ngazi zote, na kituo cha kushamirisha biashara za wanachama waaminifu.

Kuhusu suala la mlolongo wa viongozi na watawala waliopewa madaraka mbalimbali kutokana na kuwa waaminifu kwa chama-tawala, sehemu ya Zanzibar huwa naiona kama kichekesho.

Hivi kuna sababu gani hasa kwa kisiwa kisichokuwa na ukubwa wa mkoa mmoja wa Tanzania Bara (Tanganyika) kuwa na Rais, Waziri Kiongozi, Naibu Waziri Kiongozi, mawaziri dazeni na naibu mawaziri korija, makatibu wakuu wa wizara, naibu makatibu wakuu, wakurugenzi, naibu wakurugenzi, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, masheha, n.k. Inaelekea Visiwa hivyo vina viongozi wengi kuliko raia.

Lakini hata upande wa Tanzania Bara hali si tofauti sana kama tukiangalia mlololongo wa mawaziri, naibu mawaziri, makatibu wakuu na manaibu wao, wakurugenzi, wakuu wa mikoa, maofisa utawala wa mikoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa wilaya, watendaji wa tarafa na kata, hadi wenyeviti na makatibu wa vijiji.

Dhahiri, hii ni nchi inayotawaliwa kupindukia (over-governed) ingawaje maendeleo hayaonekani kwa uwiano unaofanana na ukubwa wa utawala. Dhahiri vile vile, watu wengi watakusanyika katika chombo kinachotoa fursa ya kushiriki katika hilo ‘Treni la Michuzi’ kwa sababu kuna ajira kwa ajili ya watu wengi. Hata wasiokuwa waumini wa jambo lo lote wataimba wimbo wo wote unaowahakikishia kipato kinono na maisha nafuu.

Sasa, kutokana na ukubwa wa chama, udhibiti kilichonao juu ya rasilimali za Taifa na mkusanyiko wa kimaslahi wa watu wa kila aina na tabia (silika ya kokolo), chama kimejiundia chenyewe matatizo ambayo hakikutaraji yangechukua sura iliyokuja kujitokeza. Hapa napo, kwa mara nyingine, tena, tunakutana na ile sheria ya matokeo yasiyotarajiwa (unintended consequences). Hebu tuangalie kilichotokea bila kutarajiwa.

Mwalimu Nyerere alisema kwamba hakuna mantiki ya kuwa na mfumo unaoitwa wa “vyama vingi” bila kuwa na vyama vya kweli. Wakuu wa CCM walikuwa na mawazo mengine. Walikwisha kuona jinsi walivyosumbuliwa na kile kilichoitwa G-55 wakati wa chama kimoja. Sasa, ujio wa vyama vingi uliwapa fursa ambayo waliiona kama fursa ya dhahabu.

Ni hivi: Wakati wa chama kimoja, kwa kutumia nadharia ya ubishani ndani ya chama, iliwezekana kuwa na kundi la wabunge wa chama tawala linaloipinga serikali katika masuala kadhaa na likavumiliwa, kwa sababu tulikuwa tumekumbatia nadharia ya demokrasi katika chama kimoja. Kundi la wabunge kama hao walionekana kama wanaotoa mchango muhimu katika kuifanya serikali ifanye kazi yake, na kwa maana hii lilikuwa ni kundi la upinzani usio rasmi.

Lakini baada ya kuingia katika “vyama vingi” kazi hiyo ya upinzani ilikabidhiwa rasmi kwa vyama vya upinzani, na kwa hiyo wabunge wa CCM walikuwa hawana tena nafasi ya kusimama bungeni na kukosoa serikali, hata kwa jambo ambalo hata kipofu angeona kwamba ni hovyo. Wakuu wa chama walisikika wakisema (katika kipindi cha maandalizi ya ujio wa “vyama vingi”) wakituambia baadhi yetu:

“Sasa tutawaona. Vyama vingi vinakuja, na huo ndio mwisho wenu. Ukisema fyoo dhidi ya serikali yako unapigwa ‘whip’ hata tatu. Mtakoma.”

Kwa maneno mengine nao pia walikuwa wamegundua ile sheria yangu ya matokeo yasiyotarajiwa: Kwamba lile wingu la “vyama vingi” (ambalo liliwatisha mno) lilikuwa na msitari wa fedha: Tofauti na walivyokuwa wakihofu (kwamba mfumo wa vyama vingi vingeleta demokrasia) sasa wakawa wamegundua kwamba mfumo huo ungesaidia kuua hata kale ka-demokrasia kalikokuwa kamejengeka ndani ya mfumo wa chama kimoja. Na hili wakalifanyia kazi kwa ari kubwa ili kuhakikisha kwamba “vyama vingi” maana yake ni kutokuwa na demokrasia

Walikosea sana.

Itaendelea

Raia Mwema ( Jenerali Ulimwengu)

No comments: