John MalecelaAmeanguka
WAKATI mwanasiasa mkongwe na Waziri Mkuu wa zamani, John Malecela, ameangushwa katika kuwania kuongoza Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, mageuzi yamefanyika bungeni kwa kamati zote tatu zinazosimamia matumizi ya fedha za umma, kuongozwa na wabunge wa Upinzani.
Aliyechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati mpya ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ni Mbunge wa Muleba Kaskazini, Wilson Masilingi aliyepata kura 13, akiwashinda Malecela (5) na Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Anna Abdalah (3).
Kabla ya mwaka 2006, Malecela ambaye ni Mbunge wa Mtera (CCM), alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, ambayo sasa imeunganishwa na Kamati ya Mambo ya Nje, wakati Anna Abdalah, alikuwa akiongoza Kamati ya Mambo ya Njee
John Malecela
Kwa mujibu wa habari kutoka ofisi za Bunge, awali Masilingi alitajwa kuwania kuongoza Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, akishindana na mke wa Malecela, Anne Kilango, ambaye ameshinda nafasi hiyo.
Haikuweza kufahamika mara moja sababu hasa ya Masilingi kuwania Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na kuachia Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, pamoja na kuwapo uvumi kwamba kulikua na makubaliano yasiyo rasmi kati yao.
Anne Kilango ambaye ni Mbunge wa Same Mashariki (CCM) amekuwa mwanamke mwenye kuheshimika ndani na nje ya Bunge kutokana na misimamo yake na alielezwa awali kuwa tishio katika kamati hiyo, jambo ambalo lilikuwa mtihani mkubwa kwa yeyote ambaye angeshindana naye.
Masilingi atasaidiwa na Mbunge wa Ilala (CCM), Mussa Azan Zungu, wakati Anne Kilango, atasaidiwa na Mbunge wa Mafia (CCM), Abdulkarim Shah.
Kati ya kamati tatu zilizokwenda upinzani, kamati iliyokuwa na upinzani mkali ilikua ni Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POC) ambako, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Zitto Kabwe, alimshinda Mbunge wa Wete (CUF), Mwadini Abbas Jecha, ambaye hakutarajiwa kabisa kuwania nafasi hiyo.

Wabunge wengine wa upinzani walioshinda, kama ilivyotarajiwa, ni Mbunge wa Karatu (CHADEMA), Dk. Wilbroad Slaa, aliyeshinda kuongoza Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP), John Cheyo, ambaye anaendelea kuongoza Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC).
Zitto Kabwe
Kamati nyingine ambazo zimeendelea kuongozwa na wenyeviti wa awali ni pamoja na Kamati ya Fedha na Uchumi, inayoongozwa na Mbunge wa Handeni (CCM), Dk. Abdalah Kigoda na Kamati ya Miuondombinu, inayoongozwa na Mbunge wa Singida Kusini (CCM), Mohamed Misanga.
Kamati mpya ya Nishati na Madini, imekabidhiwa kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uwekezaji na Biashara, Mbunge wa Bumbuli (CCM), William Shelukindo na aliyekuwa Makamu wake, Mbunge wa Kyela (CCM), Dk. Harison Mwakyembe, wakiwa ni wabunge waliolivalia njuga sakata la umeme wa dharura la Richmond.
Kuundwa kwa kamati hiyo, kunaelezwa kutokana na kuibuka kwa mambo mengi yanayohusiana na nishati na madini na kukabidhiwa kwa Shelukindo na Dk. Mwakyembe kumeelezwa na wabunge kuwa ni mkakati mahususi wa Bunge kulimulika zaidi eneo hilo.
Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, inaendelea kuongozwa na Mbunge wa Mpwapwa (CCM), George Lubeleje, akisaidiwa na Mbunge wa Chalinze (CCM), Ramadhani Maneno.
Aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha, Abdisalaam Issa Khatib, ameombwa na wabunge wenzake wachache waliohudhuria kikao cha kwanza kuongoza kamati ya Viwanda na Biashara akisaidiwa na Mbunge wa Mkinga (CCM), Mbaruk Mwandoro. Wajumbe wengi wa kamati hiyo wakiwamo mawaziri wa zamani na wabunge mashuhuri hawakufika kwenye uchaguzi huo.

Mbunge wa Ileje (CCM), Gideon Cheyo, ameendelea kuwa Mwenyekiti katika kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji, ambayo sasa imefanyiwa marekebisho, akisaidiwa na Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Kidawa Salehe.
Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, inaongozwa na Mbunge wa Kongwa (CCM), Job Ndugai, ambaye awali alikuwa akiongoza kamati hiyo ikiwa inahusika na Maliasili na Mazingira pekee.Lediana Mng’ong’o
Atasaidiwa na Mbunge wa Koani (CCM), Haroub Masoud wakati Kamati ya Sheria Ndogo, itaongozwa na Mbunge wa Kibakwe (CCM), George Simbachawene.Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii, anaendelea kuwa Mbunge wa Peramiho (CCM), Jenista Mhagama akisaidiwa na Mbunge wa Koani (CCM), Haroub Masoud, ambaye naye anarejea katika wadhifa wake wa awali.
Kwa hisani ya Raia Mwema.
No comments:
Post a Comment