Wednesday, April 23, 2008

Katibu Chadema, viongozi wa dini, wengine 12 watupwa rumande Buzwagi

KATIBU wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilaya ya Kahama , Lucas Petro (52) na wakazi wengine 13 , wamefikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kufanya mkusanyiko usio halali katika mgodi wa Buzwagi kushinikiza walipwe fidia.

Mratibu Msaidizi wa Polisi Mayila Kisanjo, aliwataja wengine Mahakama ya Wilaya ya Kahama mbele ya Hakimu Hassani kuwa ni Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Nyahanga, Simon Charles (45) , Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Chapulwa kupitia Chama cha Tanzania Labour (TLP), Tabo Majabi (48) na Juma Protas (40).

Mchungaji wa Kanisa la Assemblies of God (EAGT), Issa Issa (28), Mwalimu wa dini ya kiislamu Kahama Mjini, Jumanne Ntalula (48), balozi katika Kijiji cha Mwime na Mapande Machibya (56), ambaye ni mkulima kijiji cha Chapulwa.

Masanja Kashinje (50), Mathias John (45), Magaka Paulo (23), Bundala Makoye (26), Gema Maganga (41), wakazi wa Kijiji cha Mwendakulima.

Wengine ni Amos Malimi (53), mkazi wa Kijiji cha Mwime na Daudi Msuya (61), mfanyabiashara wa Kahama mjini.

Alidai kuwa washtakiwa hao wanadaiwa kufanya mkusanyiko usio halali katika lango la makao makuu ya mgodi huo, uliopo Kijiji cha Mwime kushinikizwa kulipwa fidia

Washtakiwa hao ambao walitiwa nguvuni juzi asubuhi, walikanusha mashtakana kupelekwa rumande katika Gereza la Wilaya ya Kahama hadi Mei 2, kesi yao itakapotajwa tena.

Na Zulfa Mfinanga, Shinyanga

No comments: