Wednesday, April 23, 2008

Wakazi wa Buzwagi watawanywa kwa risasi, mabomu

Familia 500 zataka kurejea katika makazi yao mgodini

WANANCHI waliohamishwa kupisha ujenzi wa Mgodi wa Buzwagi, wilayani Kahama jana walitawanywa kwa risasi na mabomu ya kutoa machozi yaliyokuwa yakipigwa na Polisi kuzima jaribio lao la kutaka kurudi kwa nguvu katika makazi yao.


Jaribio hilo ambalo lilitangazwa juzi na wananchi hao lilianza alfajiri jana
baada ya wananchi hao kukusanyika kwa wingi wakiwa na mabango mbalimbali wakitaka kurudi kwa nguvu kwenye makazi yao ambayo yapo ndani ya uzio wa Mgodi wa Buzwagi.

Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Magesa Mulongo alisema kuwa kabla ya wananchi hao kutaka kuvamia kurudi kwenye makazi yao walisambaza ujumbe kwenye simu za mikononi ikiwemo simu yake unaodai kuwa umetoka kwa mtu mwenye nguvu ya kushawishi wananchi.

Mulongo alisema katika ujumbe huo, wananchi walidai kwa kuwa hawana uwezo wa kuinunua dola(serikali) ili iwatusaidie, watadai haki yao kwa kuweka rehani damu yao na kwamba ujumbe huo ulisambazwa kwa viongozi mbalimbali wa Serikali.

Alisema wananchi hao tayari wamelipwa fidia kwa asilimia 98, lakini baada ya kutumia vibaya fedha hizo, wamerudi kudai upya kwa maelezo kwamba walipunjwa wakati wa kuingia mkataba wa fidia na Kampuni ya Barrick.

Kufuatia tukio la jana, ambapo watu14 wanashikiliwa na polisi wilayani hapa, Mulongo alifahamisha kuwa wananchi hao walivamia mgodi huo kwa lengo la kuuhujumu.

Alisema licha ya Kamati ya Ulinzi na Usalama kuwazuia kuvamia eneo hilo, waligoma kuondoka kwa madai ya kwamba mpaka Mbunge wao James Lembeli afike mgodini hapo.

Wananchi hao waliokuwa wakipiga makelele wakidai kuwa wamiliki wa mgodi huo
ni makaburu na mafisadi, walidai kuwa mbuge wao aliwaagiza kuwa warudi katika
maeneo yao ambayo tayari walikwishalipwa fedha na nyumba zao kubomolewa kupisha ujenzi wa mgodi huo.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya, kampuni ya Barrick ilikwishajenga nyumba 205 za fidia kwa wananchi walioondolewa, lakini nyumba 50 kati ya hizo bado zipo wazi baada ya wenyewe kugoma kuhamia, kwa sababu zisizoeleweka.

Mgodi huo wa Buzwagi umejumuisha vijiji vitatu, ambapo katika kijiji cha Mwendakulima tayari wote wameondoka na Mwime, familia tisa zimegoma huku zikiwa zimelipwa fidia na bado zimo ndani ya uzio wa kampuni hiyo.

Mulongo alisema kuwa katika Kijiji cha Chapulwa familia nne zimegoma kuondoka zikiwa zimelipwa fidia isipokuwa moja ambayo ilikataa kupokea.

Katika tukio la jana wananchi hao wapatao zaidi ya 500 walikuwa wamezingira lango
kuu la kuingia mgodini hapo.

Licha Mkuu Wilaya kuwata waondoke wakafanye mkutano katika ofisi za Serikali za Vijiji vyao ili kupata mwafaka wa haki zao, wananchi hao waligoma.

Baada ya kuona vurugu zinakuwa kubwa polisi waliingilia katina walianza kurusha risasi na mabomu ya kutoa hewani ili kuwatawanya wananchi.

Katika vurugu hizo watu 14 walikamatwa, lakini vinara wa vurugu hizo walitimua mbio kukwepa mkono wa sheria na polisi wanaendelea kuwasaka.

Kuanzia jana mgodi huo upo chini ya ulinzi mkali wa Jeshi la Polisi kutoka Shinyanga wakishiriana na wa wilayani Kahama.


Na Shija Felician, Kahama

No comments: