Monday, May 19, 2008

VIJANA MNATUPELEKA WAPI?

Leo katika pita pita zangu nilinasa sehemu Fulani katika foleni eneo la ilala , tulikaa pale kwa muda mrefu kidogo karibu dakika 20 , magari hayaendi huku au kule , pembeni yetu kulikuwa na vijana wamepanda nyuma ya pick up , mbele yao wakina mama wako katika basi wanaenda katika msiba .

Ghafla hawa vijana wakaanza kuimba Nambari wani eehh nambari wani ni CCM , si mnaona sasa , mikanga yenu mliyopewa hiyo wakati ule ? angalia sasa hii ndio barabara waliyoahidi , rudisheni mikanga yenu hii ndio CCM iliyowapa mikanga hiyo mkawachagua .

Wale wakina mama hawakuwa na jibu lolote , lakini walikuwa wanaogopa sana manake vijana walikuwa na hasira walikaribia mpaka kushuka katika gari walilopanda wao waende kwa wale wakina mama waliovaa zile kanga .

Hawa ni mfano wa vijana ambao kwa siku za karibuni wameonekana kulaumu chama cha mapinduzi na serikali kwa ujumla wakiona chochote mbele yao , nilitaka kuwauliza hivi ccm inahusika nini na mkandarasi aliyejenga barabara hiyo ? au ccm ndio walikagua barabara hiyo kabla yaijakabidhiwa ? yote hayo ni maswali ambayo nilitaka kuuliza .

Ni sawa na wale vijana wengine waliotiwa nguvuni kwa tuhuma za kumzomea raisi mstaafu Benjamin William mkapa kwa sababu zao binafsi , au sijui hawa vijana wanalipwa au wanapewa kitu gani mpaka wanakuwa na ujasiri wa kudhalilisha wenzao kiasi hicho .

Tabia hizi kwa kweli zinauzi na kukatisha tamaa sana , kama vijana wa leo ambao tunategemea wawe mstari wa mbele katika kujenga jamii bora zinazoangalia mbele kuanza kuzomeana njiani , kuimba nyimbo za ajabu ajabu , kuandamana katika mavyuo na mashuleni sijui kuchoma moto na kufanya vurugu nyingine .

Kwa mtindo huu vijana wasitegemee kufika popote au kusikilizwa na mtu wowote , kama mawazo yao ni kuungwa mkono na vyama vya upinzani kama wale wananchi wa tabata dampo basi watafute mengine na kama kuzomea huku , au kuimba nyimbo za kashfa hizi zinafadhiliwa na upinzani au mtu wowote yule

Waelewe nyimbo hizo na aina nyingine zozote za vitu wanavyofanya ni kuvunja sheria za jamhuri ya muugano wa Tanzania , na sheria ina mkono mrefu itakufuata popote ulipo na kukufikisha katika vyombo husika ili uweze kujibu tuhuma zinazokukabili

Vijana sasa wafanye mengine kuna mengi ya kufanya zaidi ya kuzomea , kuimba nyimbo za kashfa , kuchoma moto shule , kufanya fujo mashuleni na sehemu zingine .

Ni ushauri kutoka kwa kaka Yona Maro

No comments: