Tuesday, April 29, 2008

Membe na Chenge wavurunda mkataba Uchina

RAIS Jakaya Mrisho Kikwete ameelezwa kukerwa na jinsi mawaziri wa serikali yake wanavyofanyakazi bila uangalifu. Watu waliokaribu na Rais Kikwete na walioongozana naye katika ziara ya India, China na Marekani, waliliambia gazeti hili kuwa kukwerwa huko kulitokana na baadhi ya mawaziri kuharibu mkataba.
Walisema kuwa mkataba huo uliokuwa kwa upande mmoja usainiwe na waziri wa Tanzania na upande mwingine waziri wa China, uliharibika baada ya kusainiwa na mawaziri wawili wa Tanzania, hivyo kuharibu itifaki.
Wakizungumza kwa sharti la kutokutajwa majina gazetini, walisema kuwa mkataba huo ulikuwa batili baada ya kusainiwa na mawaziri hao waandamizi, hali iliyomfanya Rais Kikwete kuja juu kutokana na uzembe huo.Vyanzo hivyo vya habari vilidai kuwa mkataba huo ulisainiwa na mawaziri hao wawili kutokana na jinsi ulivyokuwa umeendaliwa licha ya ukweli kwamba ulikuwa ukihusu zaidi wizara moja.
Walidai kuwa mkataba huo uliokuwa ukihusisha masuala ya wizara ya miundombinu, katika mazingira yasiyoeleweka ulianza kusainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bernard Membe na kisha kusainiwa na aliyekuwa Waziri wa Miundombinu Andrew Chenge.
Vyanzo hivyo vilidai kuwa Waziri Membe alisaini mkataba huo baada ya kuwepo kwa sehemu yake ya kusaini, huku nyuma kukiwa na sehemu ya kusaini Chenge.
Kulingana na vyanzo hivyo, inadaiwa kuwa baada ya kusainiwa, mkataba huo ulikuwa batili kwa kuwa ulipaswa kuhusisha waziri mmoja wa Tanzania na mwingine wa China.
Hata hivyo haikuweza kufahamika mara moja aliyehusika na uzembe huo katika mkataba huo ambao unadaiwa uliandaliwa mapema tangu kuwapo kwa taarifa ya safari ya Rais Kikwete nchini China.
Pia haikuweza kufahamika hatua ambazo Rais Kikwete anaweza kuzichukua dhidi ya mawaziri wake hao kutokana na uzembe wa kuandaa mikataba kama ilivyojitokeza.

No comments: